×

TOSCI Yafanya Ukaguzi wa Maduka ya Mbegu Dodoma

Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imefanya ukaguzi wa maduka ya mbegu katika Wilaya za Chamwino, Mpwapwa na Dodoma DC kwa lengo la kuhakikisha wafanyabiashara wanazingatia sheria na kuuza mbegu zilizothibitishwa.

Katika ukaguzi huo, jumla ya maduka 43 yalikaguliwa ambapo maduka saba (7) yalibainika kuwa na changamoto ya kutohuisha vibali vya biashara kwa wakati, kinyume na matakwa ya Sheria ya Mbegu Sura ya 308 na kanuni zake. Kwa mujibu wa sheria, vibali hivyo vinapaswa kuhuishwa kila baada ya miaka miwili.

Wafanyabiashara waliobainika na makosa wamepewa muda wa wiki moja kuhuisha vibali vyao kupitia mfumo wa TOSCI kabla ya wakaguzi kurejea kufanya uhakiki. Hatua zaidi ikiwemo kufungia biashara itachukuliwa kwa watakaoshindwa kutekeleza maelekezo hayo.

TOSCI inaendelea kuwasihi wafanyabiashara wote wa mbegu kuzingatia sheria, kuuza mbegu zilizothibitishwa na kuhuisha vibali kwa wakati ili kulinda maslahi ya wakulima na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Leave a Comment