
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amerejeshwa rumande leo Jumatatu, Mei 25, 2026, baada ya mahakama kuahirisha shauri lake la maombi ya kuunganishwa katika kesi inayohusu mgawanyo wa mali za chama hicho hadi Juni 2, 2026, ambapo litafanyiwa usikilizwaji mbele ya Jaji David Ngunyale.
Akizungumzia hatua hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Dk Rugemeleza Nshala, amesema mahakama imeagiza upande unaopinga maombi ya mwenyekiti kuwasilisha viapo vyao ndani ya siku saba kuanzia leo kabla ya kesi hiyo kusikilizwa rasmi Juni 2, 2026 saa tano asubuhi.
Dk Nshala ameongeza kuwa hatima ya maombi hayo itategemea uamuzi wa kesi ya msingi unaotarajiwa kutolewa Mei 28, 2026, baada ya kurejeshwa Mahakama Kuu kutoka Mahakama ya Rufani. Amesema iwapo mahakama itaamua kesi hiyo bado ina nguvu kisheria, maombi ya mwenyekiti yataendelea kusikilizwa, lakini endapo itafutwa, basi maombi hayo pia yatapoteza uhalali wake.