×

Spika wa Bunge Senegal El Malick Ndiaye Atangaza Kujiuzulu

Spika wa Bunge la Senegal, El Malick Ndiaye

Spika wa Bunge la Senegal, El Malick Ndiaye ametangaza kujiuzulu wadhifa wake huku mzozo wa kisiasa ukiendelea kushika kasi nchini humo.

Hatua hiyo imefungua njia kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Ousmane Sonko kuwania nafasi ya kuongoza Bunge, siku mbili tu baada ya kufutwa kazi na Rais Bassirou Diomaye Faye.

Chama tawala cha Pastef kinachomuunga mkono Sonko kina idadi kubwa ya wabunge, jambo linaloweza kuongeza presha kwa Rais Faye ambaye tayari anakabiliwa na mgogoro wa kisiasa ndani ya serikali yake.

Aliyekuwa Waziri Mkuu, Ousmane Sonko

Wabunge wanatarajiwa kukutana Jumanne kumrejesha Sonko rasmi bungeni na kuchagua spika mpya, hatua inayoweza kuzidisha mvutano kati ya viongozi hao waliowahi kuwa washirika wa karibu kisiasa.

Mahusiano kati ya Faye na Sonko yalidorora katika miezi ya hivi karibuni baada ya Sonko kumshutumu rais huyo kwa kushindwa kuonyesha uongozi thabiti na kuchelewesha mapambano dhidi ya ufisadi uliodaiwa kufanywa na viongozi wa serikali iliyopita ya Macky Sall.

Wachambuzi wa siasa wanaonya kuwa Rais Faye anaweza kupata wakati mgumu kuendesha serikali bila uungwaji mkono wa wabunge wengi wa Pastef, huku Sonko akiendelea kuwa na ushawishi mkubwa kwa vijana na wafuasi wa chama hicho nchini Senegal.

Leave a Comment