×

Rais Samia Awaapisha Majaji Wa Mahakama Ya Rufani, Awaonya Kutenda Haki – (Picha +Video)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali mara baada ya kuwaapisha Majaji 9 wa Mahakama ya Rufani, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Mei, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewataka Majaji wa Mahakama ya Rufani aliowaapisha leo Mei 26, 2026 kutenda haki na kufanya kazi kwa uadilifu, werevu, busara pamoja na hofu ya Mungu.

Akizungumza katika hafla ya kuwaapisha majaji hao iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema Majaji wana dhamana kubwa ya kuhakikisha haki inapatikana kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

“Kwa hapa duniani ukiacha Mungu anayesimamia haki za wote, wengine ambao Mungu amewateua kusimamia haki za wote ni nyinyi Majaji katika ngazi zenu tofauti. Kwa hiyo mna dhima kubwa kwa nchi hii katika kutenda haki na kuhakikisha haki za wananchi zinapatikana,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amesema Serikali itaendelea kuimarisha uwezo wa Mahakama ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki nchini.

“Serikali itaendelea kuimarisha uwezo wa Mahakama zetu ili isimamie vizuri eneo la utoaji haki na kwa ufanisi. Mahakama zimebadilika na zimeendelea kwa kiasi kikubwa, na Mahakama ya Rufani ndiyo ngazi ya juu katika utoaji haki nchini na kila uamuzi mnaoutoa una nguvu kubwa,” amesema.

Pia amewataka majaji hao kulinda heshima na uhuru wa Mahakama huku akiwapongeza kwa uteuzi wao na kuwaasa kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya haki na maadili ya kazi yao.

Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani wakiapa Kiapo cha Maadili kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Mei, 2026.
Rais Samia akimuapisha Cyprian Phocas Mkeha kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Mei, 2026.
Rais Samia akiwa na viongozi mbalimbali kwenye picha na Majaji wa Mahakama ya Rufani, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Mei, 2026.

Leave a Comment