
Shirika la Reli Tanzania Tanzania Railways Corporation (TRC) limepiga hatua kubwa katika kuimarisha usalama wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) baada ya kununua magari maalum aina ya Ford Ranger na Mercedes-Benz Unimog yenye teknolojia ya kisasa ya laser kwa ajili ya ukaguzi wa reli.
Magari hayo yameboreshwa kuwa mfumo maalum wa Hi-Rail unaoyawezesha kufanya kazi barabarani pamoja na kwenye reli huku yakitumia mifumo ya laser kubaini hitilafu mbalimbali za reli kwa haraka na usahihi mkubwa zaidi.
Kwa mujibu wa TRC, uwekezaji huo unalenga kuongeza usalama wa safari za reli ya SGR pamoja na kuhakikisha huduma zinaendelea bila changamoto kubwa zinazoweza kusababisha ajali au usumbufu kwa wasafiri.
Magari ya Ford Ranger yanatajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya doria za haraka na kufika maeneo yenye changamoto kwa muda mfupi kutokana na uimara na uwezo wake wa kubadilika kutoka barabarani kwenda kwenye reli kwa urahisi.
Kwa upande wa Mercedes-Benz Unimog, gari hilo lina uwezo mkubwa wa kufanya kazi katika mazingira magumu huku likibeba vifaa vizito vya ukaguzi wa reli na kusaidia shughuli za kiufundi katika maeneo yenye changamoto.
Mbali na hayo, magari yote yamefungwa magurudumu maalum ya reli pamoja na mifumo ya kisasa ya laser inayoweza kuchunguza hali ya reli kwa kupima usahihi wa njia, kubaini nyufa ndogo pamoja na matatizo yasiyoonekana kwa macho ya kawaida.
Teknolojia hiyo pia ina uwezo wa kufanya ukaguzi wakati gari linaendelea kutembea kwenye reli, hali inayorahisisha ufuatiliaji wa muda halisi na kuongeza ufanisi wa kazi za ukaguzi.
Mkaguzi wa njia wa TRC, Manyama Mazula, amesema magari hayo ni sehemu muhimu ya mfumo mpya wa usalama wa reli nchini.
“Haya siyo magari ya usafiri pekee, bali ni macho yetu kwenye reli,” alisema Mazula.
Baadhi ya wasafiri wa reli ya SGR pia wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo wakisema itaongeza imani kwa usalama wa safari zao.
Akwilina Msangi ambaye ni msafiri wa mara kwa mara wa SGR alisema kuwa uwezo wa TRC kubaini matatizo mapema kabla ya ajali unatengeneza hali ya usalama zaidi kwa abiria.
Naye Zuberi Mkwama amelipongeza shirika hilo kwa uwekezaji huo akisema utaendelea kulinda usalama wa abiria pamoja na mizigo inayosafirishwa kupitia reli hiyo.
Hatua hiyo inaonyesha dhamira ya Tanzania Railways Corporation ya kuendelea kuifanya reli ya SGR kuwa ya kisasa zaidi huku Tanzania ikiendelea kuendana na viwango vya kimataifa vya usalama wa reli.