
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limetangaza kuwaita vijana 60,000 waliomaliza kidato cha sita mwaka 2026 kujiunga na mafunzo ya lazima kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni ongezeko kutoka vijana 40,000 waliokuwa wakichukuliwa awali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Mei 28, 2026 kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, Mkuu wa Utawala Tawi la JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema vijana hao wanatakiwa kuripoti makambini kuanzia Juni 1 hadi 7, 2026 kwa ajili ya kuanza mafunzo rasmi.
Mabena amesema mpango huo unawahusu wahitimu wote wa kidato cha sita kutoka shule za Tanzania Bara na Zanzibar, huku akieleza kuwa mwelekeo wa baadaye ni kuhakikisha kila kijana anayehitimu elimu hiyo anapitia mafunzo ya JKT moja kwa moja.

“Sanjari na wito huo, JKT limewapangia makambi watakaokwenda kupatiwa mafunzo na wanatakiwa kuripoti kambini kuanzia Juni 1 hadi 7, 2026,” amesema Brigedia Jenerali Mabena.
Baadhi ya makambi yaliyotajwa kupokea vijana hao ni pamoja na Rwamkoma (Mara), Msange (Tabora), Ruvu na Kibiti (Pwani), Mpwapwa na Makutupora (Dodoma), Mafinga (Iringa), Male (Ruvuma), pamoja na Mgambo na Maramba mkoani Tanga.
Makambi mengine ni Makuyuni na Oljoro (Arusha), Bulombora (Kagera), Kanembwa na Mtabila (Kigoma), Itaka (Songwe), Luwa na Milundikwa (Rukwa), Nachingwea (Lindi) pamoja na Chuo cha Uongozi cha JKT Kimbiji kilichopo Dar es Salaam.
