
Rais wa Marekani Donald Trump amesema bado hajaridhishwa na pendekezo la amani kutoka Iran licha ya siku chache zilizopita kueleza kuwa makubaliano kati ya mataifa hayo yalikuwa karibu kufikiwa.
Kauli hiyo imekuja wakati Marekani na Iran zikiendelea kushambuliana kijeshi huku juhudi za kidiplomasia zikifanyika kutafuta suluhu ya mgogoro unaoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati.
Trump amesema Iran bado inaonyesha nia ya kufanya makubaliano lakini mazungumzo yanaendelea kuwa magumu na yenye changamoto kubwa. Akizungumza katika kikao cha dharura cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu, Trump alisema Marekani bado inaamini makubaliano yanaweza kupatikana.
“Hadi sasa bado hatujaridhishwa lakini tutafikia hapo,” amesema Trump huku akidai kuwa Iran ipo katika hali ngumu kiuchumi na kijeshi.

Kauli hiyo imekuja baada ya Iran na Marekani kubadilishana mashambulizi mapya ya kijeshi, huku Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran (IRGC) likidai kulenga kambi ya kijeshi ya Marekani kufuatia mashambulizi ya Marekani dhidi ya maeneo ya Iran karibu na Bandar Abbas na eneo la Hormuz.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amesema diplomasia bado ndiyo njia kuu ya kutafuta suluhu ya mgogoro huo ingawa hali bado ni tete.
“Nafasi ya mazungumzo bado ipo na siku zijazo zitaonyesha kama pande zote mbili zitafikia maendeleo,” amesema Rubio.
Naye Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth amesema Marekani ipo tayari kutumia njia zote kuhakikisha Iran haimiliki silaha za nyuklia.