×

Wanafunzi 8 Washikiliwa Kufuatia Moto wa Shule ya Utumishi Girls Kenya

Polisi nchini Kenya wamewakamata na kuwazuilia wanafunzi wanane kuhusiana na mkasa wa moto uliotokea katika shule ya bweni ya wasichana ya Utumishi Girls Secondary School iliyopo Gilgil, Kaunti ya Nakuru.

Kupitia Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), mamlaka zimeanzisha uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha moto huo uliosababisha vifo vya wanafunzi 16.

Timu maalum ya wachunguzi imeundwa kushughulikia tukio hilo, huku uchunguzi wa vinasaba ukiendelea ili kusaidia kutambua miili ya wanafunzi waliofariki katika mkasa huo wa kutisha.

Maafisa wa polisi wameendelea kuwahoji wanafunzi, walimu pamoja na wafanyakazi wa shule hiyo huku pia wakichunguza kamera za usalama za CCTV ili kupata taarifa zaidi kuhusu chanzo cha moto huo.

Kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi, wanafunzi hao wanane wametajwa kuwa washukiwa wakuu wa tukio hilo na kwa sasa wanashikiliwa na polisi wakati uchunguzi ukiendelea.

Mamlaka nchini Kenya zimeeleza kuwa zinaendelea kuchukua maelezo kutoka kwa mashuhuda mbalimbali ili kubaini motisha ya tukio hilo la moto lililotikisa taifa hilo.

Leave a Comment