
29.05.2026, Dar es Salaam – Kampuni ya Mixx imewakabidhi zawadi washindi wa awamu ya kwanza wa kampeni ya “Kila Muamala ni Bao la Ushindi”, hatua inayokuja wakati hamasa ya mashabiki wa soka kuelekea michuano ya Kombe la Dunia ikiendelea kuongezeka nchini.
Kampeni hiyo, inayofanyika kwa ushirikiano na Hisense yenye kauli mbiu ya “Ikiingia Tu Goli”, inalenga kuwapa watumiaji wa huduma za Mixx nafasi ya kushinda zawadi mbalimbali wanapofanya miamala ya kila siku kupitia jukwaa hilo la kifedha kidijitali.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi hizo, Mkuu wa Kitengo cha Chapa na Mawasiliano – Mixx, Bi. Anisah Mamuya, alisema kampeni hiyo imebuniwa kutokana na mapenzi makubwa ya Watanzania kwa mchezo wa soka, huku ikichochea matumizi ya huduma za kifedha kidijitali.
Alisema Kombe la Dunia ni tukio linalounganisha mamilioni ya watu duniani, hivyo kampeni hiyo inalenga kuwapa Watanzania nafasi ya kushiriki msisimko huo huku wakinufaika na zawadi mbalimbali.
Katika droo ya kwanza ya kampeni hiyo, washindi saba wamejishindia fedha taslimu kiasi cha Sh milioni moja kila mmoja. Kati yao, washindi watano wanatoka Dar es Salaam, huku wawili wakitoka mikoa ya Pwani na Tanga.
Mmoja wa washindi wa fedha taslimu, Bw. Yango Kasagamba, mjasiriamali na mkazi wa Dar es Salaam, alisema zawadi ya Sh milioni moja aliyoshinda itakuwa msaada mkubwa kwake katika kuendeleza shughuli zake za kiuchumi na familia yake.
“Ninafuraha sana kuwa miongoni mwa washindi wa kampeni hii. Fedha nilizopata zitaniwezesha kuongeza mtaji katika biashara zangu za ujasiriamali na pia zitanisaidia kulipia ada ya mtoto wangu. Ninawahamasisha Watanzania kuendelea kutumia Mixx kwa sababu kila muamala unaweza kuwa fursa ya ushindi,” alisema Bw. Kasagamba.
Washindi wengine watatu walijishindia vifaa vya kielektroniki kutoka Hisense, ikijumuisha televisheni, friji na spika. Washindi hao wanatoka Dar es Salaam, Zanzibar na Tanga.
Bi. Mamuya alisema kampeni hiyo bado inaendelea na itatoa fursa kwa Watanzania wengine kushinda zawadi mbalimbali, ikiwemo fedha taslimu na vifaa vya kielektroniki kutoka Hisense.
“Bado wapo washindi watano wa kampeni ambao watapata nafasi ya kusafiri kwenda Mexico kushuhudia mechi za Kombe la Dunia mubashara na mshindi mmoja wa shilingi milioni 50 mwishoni mwa kampeni,” alisema.
Kampeni ya “Kila Muamala ni Bao la Ushindi” pia inalenga kuhamasisha matumizi ya Mixx Super App kupitia huduma mbalimbali ikiwemo kutuma fedha, kulipa bili, kufanya malipo kwa njia ya Lipa kwa Simu na miamala mingine ya kila siku.
Mixx imewahimiza Watanzania kuendelea kushiriki kampeni hiyo kwa kutumia huduma zake, ikieleza kuwa kila muamala unaofanyika unatoa nafasi ya kuingia kwenye droo za ushindi.