
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza watumishi waliohusishwa na ubadhirifu wa zaidi ya shilingi milioni 500 katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni watafutwe popote walipo, wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu huku fedha hizo zikirejeshwa serikalini.
“Wamechota fedha za wananchi. Watafutwe hata ambao walishahamishwa, popote walipo wakamatwe, wawekwe ndani na fedha za Serikali zirudi. Hii si fedha ya mtu binafsi, ni fedha ya wananchi,” alisema Dkt. Mwigulu.
Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo leo Jumamosi Mei 30, 2026 alipozungumza na wananchi wa Wilaya ya Manyoni katika Viwanja vya Tambukareli mkoani Singida akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.

Alisema taarifa alizopokea zinaonesha kuwa jumla ya zaidi ya shilingi milioni 501 zilichotwa kutoka akaunti mbalimbali za halmashauri ikiwemo Akaunti ya Maendeleo (zaidi ya shilingi milioni 213), Akaunti ya Amana (zaidi ya shilingi milioni 259) na Akaunti ya Mapato ya Ndani (zaidi ya shilingi milioni 42), jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa na Serikali.
Waziri Mkuu aliwataja watumishi wanaodaiwa kuhusika katika ubadhirifu huo kuwa ni aliyekuwa Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo Mwakapala, ambaye kwa sasa amehamishiwa mkoani Songwe, Mhasibu wa Mapato Edward Kilungu na Eliamini Maliki.

Aidha, alimwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida (RPC) kuhakikisha watumishi hao wanatafutwa, wanakamatwa na kuwekwa mahabusu hadi fedha za Serikali zitakapopatikana.
“Mweka Hazina Mwakapala arudishwe, Edward Kilungu na Eliamini Maliki watafutwe. Wakamatwe, wawekwe ndani na wasitoke mpaka fedha ya Serikali irudi,” alisema Dkt. Mwigulu.
