
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, anaripotiwa kuwasilisha ombi la kujiuzulu baada ya kudai kupokonywa mamlaka ndani ya mfumo wa uongozi wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, Pezeshkian aliieleza ofisi ya Kiongozi Mkuu wa Iran kuwa yeye pamoja na serikali yake wamekuwa wakitengwa katika maamuzi makubwa ya kitaifa jambo linalomfanya ashindwe kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Hatua hiyo imekuja wakati kukiwa na dalili za kuongezeka kwa migogoro ya madaraka ndani ya utawala wa Iran huku Marekani ikiendelea na mazungumzo na nchi hiyo kuhusu masuala ya usalama na nyuklia.
Rais wa Marekani, Donald Trump, amekuwa akizungumzia mara kwa mara mgawanyiko uliopo ndani ya uongozi wa Iran, akidai utawala huo umevurugika kwa kiwango kikubwa.
Ripoti hiyo ya kujiuzulu kwa Pezeshkian inaweza kuongeza presha mpya ndani ya siasa za Iran wakati taifa hilo likikabiliwa na changamoto za kiuchumi, kisiasa na mvutano wa kimataifa.