×

Tanzania Yatikisa Afrika, Kukipiga na Senegal Fainali AFCON U-17 Kesho

TIMU ya Taifa ya Tanzania ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, itashuka dimbani kesho Jumanne Juni 2, 2026 usiku kumenyana na Senegal katika fainali ya michuano ya TotalEnergies CAF U-17 AFCON Morocco 2026 itakayochezwa mjini Rabat, Morocco.

Mchezo huo wa fainali unatarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa Moulay El Hassan kuanzia saa 4:00 usiku kwa saa za Morocco sawa na saa 10:00 jioni kwa saa za Tanzania.

Tanzania imeandika historia kwa kufika fainali hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kuiondosha Misri kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia sare tasa ya dakika 90.

Mafanikio hayo yanaendelea kuonyesha ukuaji mkubwa wa soka la vijana nchini, hasa baada ya Tanzania kushinda mashindano ya CAF African Schools Football Championship kwa wavulana mwaka 2024 na 2025.

Kwa upande wa Senegal, walifika hatua hiyo baada ya ushindi mgumu dhidi ya wenyeji Morocco kwa penalti 7-6 kufuatia sare ya 1-1 katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa mbele ya mashabiki wengi mjini Rabat.

Sasa Tanzania itakuwa ikisaka ubingwa wake wa kwanza wa AFCON U-17 huku Senegal wakitaka kuendelea kuthibitisha ubora wao katika kukuza vipaji vya soka barani Afrika.

Kabla ya mchezo wa fainali, Morocco na Misri watacheza mchezo wa kusaka mshindi wa tatu leo Juni 1, 2026.

Timu zote nne zilizofika nusu fainali pamoja na Côte d’Ivoire, Cameroon, Mali, Algeria, Mozambique na Uganda tayari zimefuzu kushiriki Kombe la Dunia la FIFA U-17 litakalofanyika Qatar baadaye mwaka huu.

Leave a Comment