×

Kafulila: Ubunifu na Taasisi Imara Ndio Nguvu ya Uchumi wa Taifa

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP-CENTRE), David Kafulila.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP-CENTRE), David Kafulila, amesema moja ya sababu kubwa zinazoyasukuma mataifa mengi duniani kuwekeza katika mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ni kuongeza ufanisi wa taasisi za umma.

Matokeo yake, anaongeza, kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kasi.

Akizungumza leo Jumatano, Juni 3, 2026 katika mhadhara wa umma uliofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Kafulila amesema duniani kuna sababu kuu tatu zinazochochea matumizi ya mfumo wa PPP ambazo ni kuvutia mitaji ya sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya umma, kuongeza ufanisi wa taasisi na kukuza ubunifu.

Amesema tafiti zinaonesha kuwa katika baadhi ya nchi zilizoendelea, takribani asilimia 25 ya utajiri wa taifa unatokana na ufanisi wa taasisi huku rasilimali za asili zikichangia takribani asilimia tano pekee.

Kafulila ameeleza kuwa mafanikio hayo hayamaanishi kuwa nchi hizo hazina rasilimali za asili, bali zimejenga mifumo imara inayowezesha kutumia rasilimali hizo kwa tija kubwa zaidi.

“China inazalisha dhahabu nyingi kuliko nchi yoyote Afrika, Marekani ina mafuta mengi kuliko mataifa mengi duniani na Urusi ina gesi nyingi kuliko nchi yoyote Afrika. Siyo kwamba hawana rasilimali, lakini hawazioni kama msingi mkuu wa kujivunia maendeleo yao,” amesema.

Ameongeza kuwa nguvu kubwa ya mataifa hayo ipo katika rasilimali watu (human capital), ubunifu na taasisi zenye ufanisi mkubwa katika kusimamia maendeleo ya kiuchumi.

Kwa mujibu wa Kafulila, mfumo wa PPP unasaidia si tu kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo, bali pia kuimarisha ufanisi wa taasisi na kuhamasisha ubunifu ambao ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya muda mrefu ya taifa.

Leave a Comment