
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu amesema Wabunge waliokwenda Rabat, Morocco kushuhudia michuano ya AFCON U17 wakiwa na nia ya kuishabikia Timu ya Serengeti Boys hawakuwa na vibali rasmi kutoka Ofisi ya Spika.
Akizungumza leo Juni 4, 2026 Bungeni jijini Dodoma katika Bunge la Kumi na Tatu, Mkutano wa Tatu, Kikao cha Arobaini na Tatu, Zungu amesema licha ya Serikali kupitia Rais kutoa hamasa na usafiri kwa timu hiyo, baadhi ya Wabunge walijumuika kwenye msafara huo bila kufuata taratibu za kibunge.
Amesema:
“Waheshimiwa Wabunge kabla ya kuendelea, juzi kulikuwa na fainali za Under 17, Mheshimiwa Rais alitoa usafiri wa ndege na hamasa ili timu yetu ipate ushindi. Kwa bahati mbaya hatukufanikiwa.”
“Pamoja na hayo kuna Wabunge walijiunga na msafara huu kwenda Morocco. Wabunge hao hawakuwa na vibali vya Ofisi ya Spika kutoka nje ya nchi.”
Zungu ameongeza kuwa Wabunge wote husika wataandikiwa barua za kujieleza ndani ya siku nne, wakieleza kwanini walikiuka kanuni za safari za nje ya nchi bila kibali.
“Naagiza Katibu awape siku nne walete majibu yao. Wakishindwa, hatua za kinidhamu zitachukuliwa kulingana na Kanuni za Bunge,” alisisitiza Spika Zungu.