
Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kumteua Todd Blanche kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa kudumu (Attorney General), hatua inayotarajiwa kuthibitishwa na Seneti ya Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka CBS News, Blanche ambaye kwa sasa ni kaimu Mwanasheria Mkuu, amekuwa akiiongoza Idara ya Haki ya Marekani tangu Aprili mwaka huu baada ya aliyekuwa Attorney General, Pam Bondi kufutwa kazi na Trump.
Kabla ya kuteuliwa katika nafasi hiyo ya muda, Blanche aliwahi kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu na pia alikuwa mmoja wa mawakili binafsi wa Trump katika kesi mbalimbali za kisheria.
Taarifa zinaeleza kuwa Trump alitangaza nia yake ya kumteua Blanche katika hafla ya faragha iliyofanyika Ikulu ya Marekani, akisema anaamini amefanya kazi nzuri na hana mpango wa kumtafuta mgombea mwingine.
Iwapo atathibitishwa na Seneti, Blanche atakuwa mmoja wa maafisa wakuu wa Idara ya Haki katika kipindi nyeti cha kisiasa na kisheria nchini Marekani, huku akiwa amehusika pia na baadhi ya maamuzi makubwa ndani ya idara hiyo tangu kurudi kwa Trump madarakani.