
Kundi la wawekezaji kutoka Qatar lililoongozwa na Sheikh Jassim bin Hamad Al Thani halitawasilisha ofa mpya ya kuinunua Manchester United licha ya taarifa zinazoeleza kuwa baadhi ya familia ya Glazer wako tayari kuuza hisa zao katika klabu hiyo.
Sheikh Jassim aliwahi kujaribu kuinunua Manchester United mwaka 2023 baada ya familia ya Glazer kufungua milango kwa wawekezaji kuwasilisha ofa za kuinunua klabu hiyo ya Old Trafford.
Hata hivyo, jitihada hizo hazikufanikiwa baada ya bilionea wa Uingereza Jim Ratcliffe kupitia kampuni yake ya INEOS kukamilisha ununuzi wa sehemu ya hisa za klabu kwa takribani pauni bilioni 1.3.

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, baadhi ya wanafamilia wa Glazer sasa wanadaiwa kuwa tayari kuuza sehemu zao za umiliki na wanajaribu kuwashawishi wengine kufanya hivyo, jambo lililoibua tena mjadala kuhusu mustakabali wa Manchester United.
Licha ya uvumi huo, taarifa zinaeleza kuwa uwezekano wa Sheikh Jassim kurejea mezani kwa ofa mpya ni mdogo sana kutokana na namna kundi lake lilivyokatishwa tamaa katika mchakato wa awali wa mauzo.
Inaelezwa kuwa kundi hilo bado lina kumbukumbu mbaya kuhusu mazungumzo ya miaka iliyopita, hali inayofanya kurejea kwenye mbio za kuwania umiliki wa Manchester United kuwa jambo lisilopewa kipaumbele kwa sasa.