
Shirikisho la Soka Duniani, FIFA limethibitisha kuwa mwamuzi wa Somalia, Omar Abdulkadir Artan, hatachezesha mechi za Kombe la Dunia 2026 baada ya kunyimwa kuingia nchini Marekani.
Kwa mujibu wa FIFA, Artan hataweza kufanya mazoezi wala kuchezesha mashindano hayo kufuatia uamuzi wa mamlaka za Marekani kutomruhusu kuingia nchini humo, licha ya kuripotiwa kuwa alikuwa na visa halali ya kusafiria.
FIFA pia imesema haihusiki na taratibu za uhamiaji za nchi mwenyeji, ikiwemo maamuzi ya utoaji visa, na tatizo lake halitashugulikiwa kwa sasa.

Artan alikuwa ameandika historia kuwa mwamuzi wa kwanza kutoka Somalia kuchaguliwa kuchezesha Kombe la Dunia, baada ya kutajwa miongoni mwa waamuzi 52 wa michuano hiyo ya 2026.
Tukio hilo limezua mjadala mkubwa kimataifa, huku baadhi ya wadau wakihusisha suala hilo na sera kali za uhamiaji za Marekani dhidi ya baadhi ya mataifa, yakiwemo Somalia.