×

Trump: Makubaliano ya Amani Iran na Israel Yamefikia Hatua za Mwisho

Rais wa Marekani Donald Trump

Rais wa Marekani Donald Trump amesema mazungumzo ya amani kati ya Iran na Israel yako katika hatua za mwisho baada ya pande hizo kusitisha mashambulizi mapya yaliyokuwa yakihatarisha kurejea kwa vita vikubwa vya Mashariki ya Kati.

Trump alisema wapatanishi wanaelekea kufikia makubaliano mazuri sana ndani ya siku mbili hadi tatu zijazo, akidai Marekani imechangia kuzuia mapigano zaidi kati ya Iran na Israel.

Hata hivyo, hali bado imeendelea kuwa ya tahadhari baada ya Iran na Israel kurushiana makombora katika siku za hivi karibuni licha ya kuwepo kwa usitishaji vita tangu Aprili 8. Iran imesisitiza kuwa makubaliano yoyote lazima yahusishe pia vita vya Lebanon ambako Israel inaendelea kupambana na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Tehran.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema nchi yake itaendelea kujilinda dhidi ya mashambulizi yoyote, huku Waziri wa Ulinzi Israel Katz akisisitiza operesheni za kijeshi kusini mwa Lebanon zitaendelea.

Kwa mujibu wa ripoti ya Axios, Trump alimwonya Netanyahu dhidi ya kuongeza mashambulizi makubwa dhidi ya Iran, akisema Israel inaweza kujikuta peke yake endapo itapuuzia msimamo wa Marekani wa kutaka utulivu.

Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance pia amesema licha ya Marekani na Israel kuwa washirika wakubwa, kuna maeneo ambayo maslahi yao yanatofautiana.

Wakati huo huo, mashambulizi ya Israel kusini mwa Lebanon yameripotiwa kuua watu wasiopungua 14 kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Lebanon.

Licha ya mvutano huo, maisha katika mji mkuu wa Iran, Tehran yameonekana kurejea taratibu huku wananchi wakiendelea na shughuli zao kwa tahadhari kubwa.

Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema Tehran bado ipo mezani kwa ajili ya mazungumzo ya kidiplomasia huku Pakistan ikiendelea na juhudi za upatanishi katika mgogoro huo.

MBUNGE SHIGONGO AMLIZA MAMA ALIYEMWAMBIA AENDE BENKI AKACHUKUE PESA – ASEMA ALIDHANI UTANI…

Leave a Comment