×

Rais Samia Aongoza Mapokezi ya Rais wa Singapore Ikulu ya Dar (Picha +Video)

Rais wa Jamhuri ya Singapore,  Tharman Shanmugaratnam, amewasili nchini kwa ziara ya Kitaifa ya siku 3, kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amempokea rasmi Tharman Shanmugaratnam katika Ikulu ya Dar es Salaam mara baada ya kuwasili nchini kwa ziara ya kitaifa inayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Singapore.

Katika mapokezi hayo yaliyofanyika Juni 09, 2026, viongozi hao wawili walionekana wakisalimiana kwa furaha kabla ya kuanza mazungumzo rasmi kuhusu maeneo mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo biashara, uwekezaji, uchumi, teknolojia na maendeleo ya miundombinu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Singapore, Mheshimiwa Tharman Shanmugaratnam mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa Ziara ya Kitaifa, tarehe 09 Juni, 2026.

Ziara ya Rais wa Singapore nchini Tanzania inaelezwa kuwa sehemu ya juhudi za kuendeleza ushirikiano wa kimataifa na kufungua fursa mpya za kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.

Singapore ni miongoni mwa nchi zinazotajwa kuwa na maendeleo makubwa katika sekta za biashara, bandari, usafirishaji na teknolojia, huku Tanzania ikiendelea kuvutia wawekezaji wa kimataifa kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Wananchi na wadau mbalimbali wameendelea kufuatilia kwa karibu ziara hiyo wakiamini inaweza kuleta matokeo chanya katika ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo kati ya Tanzania na Singapore.

Tharman Shanmugaratnam akikagua gwaride la heshima la mapokezi mara baada ya kuwasili Ikulu.
Rais Tharman Shanmugaratnam ameweka historia ya kuwa Rais wa kwanza kutembelea nchini tangu kuanzishwa kwa mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1980.

Leave a Comment