
Serikali ya Somalia imemtetea mwamuzi wake maarufu Omar Artan baada ya kunyimwa ruhusa ya kuingia Marekani, jambo lililomfanya kushindwa kuwa mwamuzi wa kwanza kutoka Somalia kuchezesha michuano ya Kombe la Dunia.
Kupitia taarifa iliyotolewa Jumanne, Wizara ya Michezo ya Somalia ilieleza masikitiko yake makubwa kuhusu tukio hilo, ikisema licha ya juhudi za kidiplomasia zilizofanywa pamoja na Shirikisho la Soka Duniani, FIFA, haikuwezekana kupata suluhisho chanya.
Artan, ambaye ni mwamuzi aliyewahi kushinda tuzo mbalimbali, alizuiwa kuingia Marekani Jumamosi baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami. Mamlaka ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani zilisema alinyimwa kuingia baada ya ukaguzi wa kawaida.
Mwamuzi huyo alikuwa miongoni mwa waamuzi 52 walioteuliwa na FIFA kuchezesha Kombe la Dunia 2026 litakalofanyika Marekani, Canada na Mexico.
Somalia imesema inaendelea kumuunga mkono Artan na ina imani kubwa na uadilifu pamoja na taaluma yake katika maendeleo ya soka nchini humo na kimataifa.
FIFA pia imethibitisha kuwa Artan hatashiriki kwenye mashindano hayo yatakayoanza Alhamisi hii.
Tukio hilo limeibua mjadala mkubwa, hasa kutokana na Somalia kuwa miongoni mwa nchi zilizowekwa kwenye orodha ya vizuizi vya safari chini ya sera za uhamiaji za utawala wa Donald Trump.