×

Marekani Yaishambulia Iran Tena, Trump Atoa Onyo Kali

Jeshi la Marekani limesema Alhamisi limefanya mashambulizi mapya dhidi ya malengo ya kijeshi ya Iran, baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuonya kwamba Tehran itakabiliwa na mashambulizi makali iwapo jitihada za kufikia makubaliano ya amani zitashindikana.

Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) imesema vikosi vyake vilifanya mashambulizi mengine ya kujilinda kwa maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu wa Marekani.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao yake rasmi ya kijamii, CENTCOM ilisema kuwa vikosi vya Marekani vililenga mifumo ya mawasiliano pamoja na maeneo ya ulinzi wa anga katika maeneo mbalimbali ya Iran mapema Alhamisi.

Kamandi hiyo ilieleza kuwa vikosi vya Jeshi la Wanamaji, Jeshi la Anga na Jeshi la Majini la Marekani vilitumia silaha za kisasa zenye uwezo wa kulenga shabaha kwa usahihi dhidi ya maeneo yaliyotajwa kuwa tishio kwa wanajeshi wa Marekani na meli za biashara zinazopita katika maji ya eneo hilo.

“Mashambulizi haya ni jibu kwa vitendo vya uchokozi vinavyoendelea kutoka Iran, ilisema CENTCOM, ikiongeza kuwa vikosi vya Marekani viko macho, vina uwezo mkubwa wa kijeshi na viko tayari wakati wowote.

Awali, CENTCOM ilitangaza kuwa mashambulizi hayo ya kujilinda yalianza saa 6:15 usiku kwa saa za Kiarabu (AST), yakilenga malengo kadhaa ndani ya Iran.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House, Trump alisema Marekani itaendelea na operesheni za kijeshi huku ikiendelea kutafuta suluhisho la kidiplomasia.

“Tutakuwa tukiwashambulia, tutawashambulia kwa nguvu sana,” alisema Trump, akirejea tukio la kudunguliwa kwa helikopta ya Marekani aina ya Apache katika Mlango wa Hormuz.

Rais huyo alisema Washington bado imejizatiti kufikia makubaliano na Tehran.

“Tunataka makubaliano yenye maana na yanayoweza kufanya kazi,” alisema Trump.

Aliongeza kuwa Iran tayari imekubali kimsingi kutotengeneza silaha za nyuklia, lakini makubaliano ya mwisho bado hayajasainiwa rasmi.

Trump pia alidai kuwa Marekani imekuwa ikiondoa kwa siri mamilioni ya mapipa ya mafuta kutoka Iran, akisema hatua hiyo imechangia kuzuia kupanda kwa bei za mafuta duniani.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, alisema Iran haitakuwa na busara kuendelea kuichokoza Marekani kufuatia mashambulizi hayo mapya.

“Kwa sasa haya ni mashambulizi ya kujilinda ili kuhakikisha tunawalinda watu wetu,” alisema Hegseth akiwa katika ziara kwenye kambi ya kijeshi ya Marekani ya Guantanamo Bay nchini Cuba.

Hegseth alisisitiza kuwa Trump bado analenga kufanikisha makubaliano yatakayozuia kabisa Iran kupata silaha za nyuklia.

“Rais Trump anatafuta makubaliano. Lakini si makubaliano ya kawaida, bali makubaliano bora kwa niaba ya wananchi wa Marekani ili kuhakikisha Iran haipati silaha za nyuklia,” alisema.

Leave a Comment