
Mvutano kati ya Iran na Marekani umeongezeka kwa kasi baada ya Iran kutangaza kufunga kabisa Mlango wa Hormuz, mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani.
Hatua hiyo imetangazwa kufuatia mashambulizi mapya ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani dhidi ya malengo ya kijeshi ya Iran, hali iliyosababisha ongezeko kubwa la taharuki katika masoko ya kimataifa ya nishati.
Kwa mujibu wa taarifa ya uongozi wa juu wa kijeshi wa Iran, amri hiyo inamaanisha kuwa meli zote za mafuta na za biashara hazitaruhusiwa kupita katika eneo hilo nyeti, na onyo limetolewa kuwa zitashambuliwa endapo zitajaribu kuvuka.
Mlango wa Hormuz ni njia ya kimkakati inayotumiwa kusafirisha sehemu kubwa ya mafuta kutoka nchi za Ghuba kuelekea masoko ya Asia, Ulaya na maeneo mengine duniani, hivyo uamuzi huo una athari kubwa kwa uchumi wa dunia.

Kufuatia tangazo hilo, bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa ilipanda kwa muda mfupi, ambapo Brent crude ilikaribia dola 93 kwa pipa na West Texas Intermediate (WTI) ikafikia takriban dola 90 kwa pipa kabla ya kurejea katika hali ya utulivu wa muda.
Wachambuzi wa masoko wanasema wafanyabiashara sasa wanasubiri kuona kama Iran itatekeleza kikamilifu uamuzi huo au kama ni sehemu ya mkakati wa kuongeza shinikizo la kidiplomasia katika mgogoro unaoendelea na Marekani.
Mgogoro huo unaendelea kuzua wasiwasi mkubwa duniani kutokana na umuhimu wa Mlango wa Hormuz katika uchumi wa mafuta na usafirishaji wa kimataifa.