
Rais wa Marekani Donald Trump ameongeza kauli zake kali kuhusu uwezekano wa kukiteka Kisiwa cha Kharg cha Iran, akisema Marekani inaweza kukichukua katika siku zijazo ili kudhibiti kwa kiwango kikubwa soko la mafuta na gesi la taifa hilo la Mashariki ya Kati.
Katika mahojiano na Fox News, Trump alisema angependa kukichukua kisiwa hicho kwa sababu kinaweza kuingizia Marekani mapato makubwa, lakini akakiri kuwa operesheni ya kijeshi ya ardhini itakuwa ngumu na yenye gharama kubwa.
“Sipendi kupeleka wanajeshi ardhini, lakini ningependa kukichukua kwa sababu kina thamani kubwa sana,” alisema Trump.
Kisiwa cha Kharg kinatajwa kuwa moyo wa sekta ya mafuta ya Iran, kwani takribani asilimia 90 ya mafuta ghafi yanayosafirishwa nje ya nchi hupitia katika kituo hicho. Kisiwa hicho kiko karibu na mwambao wa Iran katika Ghuba ya Uajemi na kina miundombinu mikubwa ya kupakia mafuta kwenye meli za kimataifa.
Mwezi Machi, jeshi la Marekani lilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya malengo ya kijeshi yaliyopo katika kisiwa hicho. Trump alidai kuwa mashambulizi hayo yaliharibu vituo vingi vya kijeshi, lakini miundombinu ya mafuta iliachwa bila kushambuliwa ili kuepusha madhara makubwa ya kiuchumi.
Licha ya vitisho hivyo, wataalamu wa masuala ya kijeshi wameonya kuwa jaribio lolote la kukiteka Kisiwa cha Kharg linaweza kuupanua zaidi mzozo kati ya Marekani na Iran badala ya kuumaliza.
Aliyekuwa kamanda wa Jeshi la Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, Joseph Votel, alisema operesheni hiyo ingehitaji mamia ya wanajeshi pamoja na msaada mkubwa wa vifaa na usafirishaji, huku wanajeshi hao wakikabiliwa na hatari kubwa ya mashambulizi.
Kwa upande wake, Iran imeimarisha ulinzi wa kisiwa hicho kwa kuongeza wanajeshi, mifumo ya makombora ya kujihami na mabomu ya ardhini katika maeneo yanayokizunguka.
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, ameonya kuwa vikosi vya Iran viko tayari kujibu kwa nguvu yoyote iwapo Marekani itajaribu kuingia katika eneo hilo.
Hata hivyo, wakati mvutano ukiendelea, Trump hivi karibuni alitangaza kusitisha mashambulizi mapya ya anga dhidi ya Iran akidai kuwa kuna maendeleo katika mazungumzo ya kidiplomasia kati ya Washington na Tehran.
Kauli hizo zinaendelea kuongeza wasiwasi wa jumuiya ya kimataifa kuhusu mustakabali wa usalama katika Ghuba ya Uajemi, eneo muhimu kwa biashara ya mafuta duniani.