×

Makamu wa Rais JD Vance Afichua Masharti Ya Makubaliano na Iran

Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance.

Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amesema Rais wa Marekani, Donald Trump, huenda akayatoa hadharani makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na Iran kabla ya Ijumaa, huku kusainiwa rasmi kwa ana kwa ana kukitarajiwa kufanyika nchini Uswisi.

Akizungumza na vyombo vya habari akiwa nchini Ufaransa kabla ya mkutano wa viongozi wa G7, Trump alisema makubaliano hayo tayari yamesainiwa kwa njia ya kielektroniki na viongozi wa Marekani na Iran, na kwamba maandishi yake yatawekwa wazi muda mfupi baada ya hafla ya kusainiwa rasmi.

Trump pia alisema kuwa njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani ya Mlango wa Hormuz  umeanza kufunguliwa kwa sehemu na unatarajiwa kufunguliwa kikamilifu kufikia Ijumaa.

Kwa upande wake, Vance alisisitiza kuwa Iran haitapokea fedha yoyote kutokana na kusaini makubaliano hayo. Alieleza kuwa kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi kutategemea hatua zitakazothibitishwa za Iran, ikiwemo kupunguza akiba yake ya urani iliyoboreshwa na kuruhusu ukaguzi wa kimataifa wa mpango wake wa nyuklia.

“Iwapo Iran itachukua hatua zinazoweza kuthibitishwa za kuondoa akiba ya urani iliyoboreshwa na kuruhusu mfumo wa ukaguzi unaohitajika, basi nafuu ya vikwazo itafuata,” alisema Vance.

Aidha, alibainisha kuwa Marekani inatarajia Mlango wa Hormuz kuendelea kuwa wazi kwa muda mrefu bila kutozwa ushuru wa kupita, huku mazungumzo yakiendelea ili kukamilisha vipengele mbalimbali vya makubaliano hayo.

Makubaliano hayo yanatajwa kuwa hatua kubwa zaidi kuelekea kumaliza mzozo kati ya Marekani, Israel na Iran uliosababisha vifo vya maelfu ya watu na kuyumbisha masoko ya nishati tangu ulipoanza kufuatia mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran mwezi Februari mwaka huu.

Hata hivyo, bado kuna masuala muhimu yanayohitaji kujadiliwa, ikiwemo mustakabali wa mpango wa nyuklia wa Iran na hali ya usalama katika eneo la Mashariki ya Kati.

Leave a Comment