Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa benki ya NMB, Ruth Zaipuna (katikati), akiwa na Menejimenti Kuu ya benki hiyo wakionyesha ishara ya furaha mara baada ya uzinduzi wa NMB Mkononi Super App.
Kupitia jukwaa hilo, wateja wataweza kupata huduma za mikopo, bima, uwekezaji, malipo, huduma za vikundi pamoja na ununuzi wa bando la mawasiliano bila ulazima wa kutembelea matawi ya benki kwa huduma za kawaida.
Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (kushoto), akijaribu huduma za NMB Mkononi Super App wakati wa uzinduzi wake. Anayemwelekeza kwa kutumia iPad ni Mtaalamu wa Bima wa NMB, Sangwani Mkandawile (katikati).
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB Bank Plc, Ruth Zaipuna, alisema kuwa NMB Mkononi Super App ni zaidi ya programu ya kibenki, bali ni jukwaa la fursa na uwezeshaji linalolenga kuwahudumia makundi mbalimbali ya Watanzania.
“Jukwaa hili limeundwa kuwawezesha wanafunzi, wafanyakazi, wakulima, wafanyabiashara, wajasiriamali na wawekezaji kusimamia mahitaji yao ya kifedha kwa urahisi kupitia simu zao za mkononi,” alisema Zaipuna.
Katika hatua ya kuongeza upatikanaji wa mitaji, NMB imesema wateja binafsi wanaokidhi vigezo wataweza kuomba mikopo ya hadi Shilingi milioni mbili kupitia programu hiyo, huku wafanyabiashara wadogo wanaostahili wakipata mikopo ya hadi Shilingi milioni tano.
Hata hivyo, wataalamu wa sekta ya fedha wanaona kuwa ongezeko la upatikanaji wa mikopo kidijitali linaifanya elimu ya fedha kuwa muhimu zaidi, hasa katika kuwawezesha wananchi kuelewa gharama za mikopo, masharti ya mikataba, muda wa marejesho na uwezo wao wa kulipa kabla ya kukopa.
Uzinduzi wa NMB Mkononi Super App unaashiria hatua nyingine muhimu katika safari ya mageuzi ya kidijitali ya sekta ya benki nchini Tanzania, huku ukionyesha namna teknolojia inavyoendelea kubadilisha upatikanaji na matumizi ya huduma za kifedha kwa wananchi wa kada mbalimbali.