×

Diddy Apunguziwa Kifungo kwa Mara Nyingine, Kuachiwa 2028

Msanii na mfanyabiashara maarufu wa muziki Sean Combs.

Rapa na mfanyabiashara maarufu wa Marekani, Sean ‘Diddy’ Combs, ameongezewa matumaini ya kutoka gerezani mapema zaidi baada ya tarehe yake ya kuachiwa huru kusogezwa mbele kwa mara nyingine huku rufaa yake ikiendelea kusikilizwa mahakamani.

Kwa mujibu wa taarifa za Ofisi ya Magereza ya Marekani, Diddy sasa anatarajiwa kuachiwa kutoka gereza la shirikisho mnamo Februari 23, 2028. Hii ni baada ya tarehe hiyo kubadilishwa mara kadhaa katika miezi ya hivi karibuni. Awali alikuwa anatarajiwa kuachiwa Aprili 15, 2028, kabla ya tarehe hiyo kusogezwa kutoka Aprili 25 na hapo awali Juni 4, 2028.

Ingawa mamlaka za magereza hazijatoa maelezo rasmi kuhusu mabadiliko hayo, Diddy kwa sasa anashiriki programu maalumu ya matibabu na urekebishaji wa matumizi ya dawa za kulevya katika gereza la FCI Fort Dix, jimbo la New Jersey. Mawakili wake waliomba apelekwe katika gereza hilo kutokana na uwepo wa programu za matibabu na ukaribu wake na familia.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 56 anatumikia kifungo cha miezi 50 jela baada ya kupatikana na hatia mwaka jana kwa makosa mawili ya kusafirisha watu kwa ajili ya kujihusisha na ukahaba. Hata hivyo, aliachiliwa huru katika mashtaka mengine mazito zaidi yaliyohusisha biashara ya ngono na kula njama za uhalifu.

Mawakili wa Diddy waliwasilisha rufaa dhidi ya hukumu na kifungo chake mwezi Desemba mwaka jana wakidai kuwa mahusiano yaliyotajwa katika kesi hiyo yalikuwa ya ridhaa na kwamba adhabu aliyopewa ilikuwa kubwa kupita kiasi.

Katika nyaraka za rufaa zilizowasilishwa mwezi Machi, upande wa utetezi uliieleza hukumu hiyo kuwa ni “upotoshaji wa haki” na kuomba kuachiliwa kwake mara moja au kesi irejeshwe mahakamani kwa ajili ya kupangiwa upya adhabu.

Hata hivyo, waendesha mashtaka wa serikali ya Marekani wameiomba mahakama ya rufaa kutupilia mbali hoja hizo wakisisitiza kuwa jaji aliyetoa hukumu alizingatia ushahidi wote uliowasilishwa wakati wa kesi.

Rufaa hiyo bado ipo mbele ya Mahakama ya Rufaa ya Marekani ya Mzunguko wa Pili, jambo linalomaanisha kuwa vita vya kisheria vya Diddy bado havijafikia mwisho licha ya tarehe yake ya kuachiwa gerezani kusogezwa mbele.

Leave a Comment