×

Trump: Mlango wa Hormuz Kufunguliwa Kikamilifu Ndani ya Siku Mbili

Rais wa Marekani, Donald Trump leo Juni 17, 2026 amesema anatarajia njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani, katika mlango wa bahari wa Hormuz, kufunguliwa kikamilifu ndani ya siku mbili zijazo kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na Iran.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa viongozi wa mataifa makubwa duniani wa G7 Summit, Trump alisema makubaliano hayo ni yenye nguvu na yameleta matumaini makubwa kwa masoko ya dunia.

“Njia ya Hormuz tayari imefunguliwa kwa kiasi na itafunguliwa kikamilifu ndani ya siku moja au mbili zijazo,” alisema Trump.

Trump alieleza kuwa masoko ya fedha yameonyesha mwitikio chanya tangu kutangazwa kwa hati ya makubaliano (memorandum of understanding) kati ya Marekani na Iran, akidai kuwa thamani za masoko zimeongezeka kwa kiwango kikubwa katika siku za hivi karibuni.

Pia aligusia kushuka kwa bei ya mafuta duniani, akisema bei ya mafuta ghafi imeshuka hadi kati ya dola 73 na 74 kwa pipa, karibu na viwango vilivyokuwepo kabla ya kuanza kwa mgogoro huo.

Kwa mujibu wa Trump, kufunguliwa kwa Mlango wa Hormuz ni hatua muhimu kwa uchumi wa dunia kwa sababu njia hiyo hupitisha sehemu kubwa ya mafuta yanayosafirishwa kimataifa.

Leave a Comment