
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeandika historia nyingine baada ya kufanikisha salama uzazi wa watoto watano kwa wakati mmoja kwa mama mmoja mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam.
Mama huyo, Bi. Victoria Mkwizu, alijifungua watoto hao watano Juni 13, 2026 katika hospitali hiyo, ambapo watoto wote pamoja na mama yao wanaendelea vizuri chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya.
Kwa mujibu wa taarifa ya Muhimbili, watoto hao watano wanajumuisha wavulana watatu na wasichana wawili. Uzazi huo wa kipekee ulifanikishwa kupitia huduma maalumu zilizotolewa na timu ya madaktari bingwa, wauguzi na wataalamu wengine wa afya wa hospitali hiyo.

Akizungumza akiwa wodini, Bi. Victoria alieleza shukrani zake kwa madaktari na wauguzi wa Muhimbili kwa huduma bora na uangalizi wa karibu alioupata tangu alipolazwa hadi alipofanikiwa kujifungua salama.
“Ninawashukuru sana madaktari, wauguzi na wataalamu wote wa afya wa Muhimbili kwa namna walivyonihudumia kwa upendo na weledi mkubwa. Uangalizi wao umewezesha mimi na watoto wangu kuwa salama na kuendelea vizuri,” alisema.
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Rachel Mhaville, alisema tukio hilo ni la kipekee na lilihitaji maandalizi pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa wataalamu ili kuhakikisha usalama wa mama na watoto hao.

“Huu ni uzazi wa kipekee ambao umehitaji maandalizi na ufuatiliaji wa karibu kutoka kwa wataalamu wetu. Tunampongeza Bi. Victoria kwa kujifungua salama na tunawatakia yeye pamoja na watoto wake afya njema,” alisema Dkt. Mhaville.
Aidha, hospitali hiyo imetangaza kugharamia gharama zote za matibabu za mama huyo na watoto wake kuanzia alipolazwa Mei 15, 2026 hadi watakapomaliza matibabu na kuruhusiwa kurejea nyumbani.
Muhimbili imesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha mama na watoto hao wanaendelea kupata huduma bora za afya katika kipindi hiki muhimu baada ya kujifungua.