×

Mwigulu: Hakuna Ubaguzi wa Huduma za Afya Kati ya Bara na Zanzibar – Video

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, amesema huduma za afya zinazotolewa nchini hazibagui wananchi kwa kuzingatia upande wa Muungano wanaotoka, bali kinachoangaliwa ni uwepo wa bima ya afya inayotambulika ili kupata huduma stahiki.

Akijibu swali la papo kwa papo kutoka kwa Mbunge wa Segerea, Agnesta Kaiza, Bungeni jijini Dodoma Juni 18, 2026, Waziri Mkuu alisema kuwa hakuna changamoto ya kimahusiano kuhusu matumizi ya rasilimali au utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano.

“Kuhusu ngazi ya matibabu, hakiangaliwi umetokea upande gani wa Muungano. Kinachoangaliwa ni kama una kadi ya bima inayotambulika ili uweze kupata huduma. Hii ni kwa pande zote za Muungano na hatuna tatizo la kimahusiano kuhusu matumizi ya rasilimali wala utoaji wa huduma,” alisema Dkt. Nchemba.

Alifafanua kuwa Serikali imeweka mifumo inayowezesha Watanzania kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kupata huduma mbalimbali kwa kuzingatia taratibu na sheria zilizopo, huku ushirikiano kati ya pande hizo mbili ukiendelea kuimarika katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu na huduma za kijamii.

Kauli hiyo ilikuja katika mjadala uliohusu utaratibu wa kisera na kisheria wa kuwahudumia Watanzania wa pande zote za Muungano katika masuala yasiyo ya Muungano, ikiwemo huduma za afya.

Leave a Comment