
Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania Juni 19, 2026 kwa ziara ya kitaifa, ikiwa ni ziara yake ya pili nchini tangu alipoingia madarakani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Juni 18, 2026 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu, ziara hiyo inaendelea kuimarisha uhusiano wa kindugu na wa kihistoria kati ya Tanzania na Namibia, uliojengwa katika misingi ya harakati za ukombozi wa Afrika, mshikamano na ushirikiano wa maendeleo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Juni 20, 2026, Rais Nandi-Ndaitwah atafanya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika Ikulu ya Dar es Salaam. Mazungumzo hayo yanatarajiwa kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa pande mbili pamoja na masuala ya kikanda na kimataifa yenye maslahi ya pamoja.

Baada ya mazungumzo hayo, viongozi hao wawili wanatarajiwa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu matokeo ya vikao vyao na mwelekeo wa ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.
Akiwa nchini, Rais Nandi-Ndaitwah pia atatembelea eneo la Magomeni Mwembechai jijini Dar es Salaam, ambako aliwahi kuishi katika miaka ya 1980 alipokuwa Mwakilishi Mkuu wa chama cha South West Africa People’s Organization (SWAPO). Ziara hiyo inatajwa kuwa na umuhimu mkubwa wa kihistoria kutokana na mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Namibia.
Vilevile, kiongozi huyo atatembelea Kambi ya Wapigania Uhuru wa Harakati za Ukombozi Barani Afrika iliyopo Kongwa, kabla ya kuhitimisha ziara yake nchini Juni 22, 2026.
