
Nahodha wa Cristiano Ronaldo ameripotiwa kuahidi kuwazawadia wachezaji wenzake wa timu ya Taifa ya Ureno magari mapya ya kifahari aina ya Rolls-Royce Phantom iwapo watafanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia 2026.
Taarifa hizo zilizosambaa kwa kasi mitandaoni zinadai kuwa kila mchezaji atapata gari lenye thamani ya takribani dola 580,000 za Marekani endapo watabeba taji hilo.
Hata hivyo, hadi sasa hakuna uthibitisho rasmi kutoka kwa Ronaldo mwenyewe wala kutoka Shirikisho la Soka la Ureno kuhusu madai hayo. Ripoti mbalimbali zimeeleza kuwa habari hiyo bado haijathibitishwa na inaonekana kusambazwa zaidi kupitia mitandao ya kijamii kuliko vyanzo rasmi.
Ronaldo, mwenye miaka 41, kwa sasa anacheza Kombe la Dunia la sita katika historia yake akiwa nahodha wa Ureno na anafukuzia ndoto ya kutwaa taji la dunia kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya soka.
Ingawa simulizi hiyo imevutia mashabiki wengi duniani kutokana na ukubwa wa zawadi inayodaiwa kutolewa, kwa sasa inapaswa kutazamwa kama taarifa ambayo haijathibitishwa rasmi mpaka pale itakapotolewa tamko kutoka kwa Ronaldo au mamlaka husika.
