
Klabu ya Manchester United imepiga hatua kubwa katika mpango wake wa kujenga uwanja mpya wa kisasa wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 100,000 baada ya kuthibitisha kuwa tayari imepata sehemu kubwa ya ardhi inayohitajika kwa mradi huo mkubwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumatatu, klabu hiyo ya Ligi Kuu Uingereza, Manchester United imefanikiwa kupata eneo la ekari 25 lililopo takribani mita 350 kutoka uwanja wa kihistoria wa Old Trafford, eneo ambalo litakuwa msingi wa ujenzi wa uwanja mpya.
Eneo hilo limenunuliwa kutoka kwa kampuni ya Indurent pamoja na kampuni inayomilikiwa na Blackstone, hatua inayoashiria kuanza kwa kasi kwa mradi unaokadiriwa kugharimu takribani pauni bilioni 2 (sawa na dola bilioni 2.65).
Uwanja huo mpya unapangwa kujengwa karibu kabisa na Old Trafford ili kulinda historia na utamaduni wa klabu hiyo, ambayo imekuwa nyumbani kwa Manchester United tangu mwaka 1910.
Mkurugenzi Mtendaji wa mradi wa uwanja mpya, Collette Roche, amesema lengo ni kujenga uwanja wa kiwango cha dunia huku mashabiki wakiwa sehemu ya maamuzi muhimu.
Amesema: “Tumejizatiti kujenga uwanja wa kisasa kwa ushirikiano na mashabiki wetu, si kwa ajili yao tu, bali pamoja nao, huku tukizingatia mazingira ya ushabiki, uwezo wa kumudu bei na urahisi wa kufika.”
Old Trafford, ambayo ina uwezo wa kuchukua zaidi ya mashabiki 74,000, haijafanyiwa maboresho makubwa tangu mwaka 2006, na kwa miaka ya hivi karibuni imekumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuvuja kwa paa, mifumo duni ya maji na hata taarifa za panya.
Mwekezaji mdogo Jim Ratcliffe, ambaye anamiliki takribani asilimia 29 ya klabu na kusimamia masuala ya soka, amekuwa akipendelea ujenzi wa uwanja mpya badala ya ukarabati wa Old Trafford.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa klabu hiyo Omar Berrada alieleza kuwa uwekezaji mkubwa katika mradi huu unaweza kuathiri bajeti ya usajili na ushindani wa timu kwa kipindi cha takribani miaka mitano.
Hata hivyo, licha ya changamoto za ndani na nje ya uwanja, Manchester United inaendelea kujipanga upya baada ya misimu ya kuyumba, huku ikifanikiwa kumaliza nafasi ya tatu katika msimu uliomalizika na kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza katika misimu miwili.
Mashabiki sasa wanasubiri kuona kama mradi huu mkubwa utaibadilisha klabu hiyo kurejea kwenye enzi zake za mafanikio ya kihistoria.