×

Uchaguzi Mkuu wa Kenya Kufanyika Agosti 10, 2027, Ratiba Kamili Yawekwa Wazi

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) imetangaza rasmi kuwa Uchaguzi Mkuu wa Kenya utafanyika Jumanne, Agosti 10, 2027, huku ikitoa ratiba ya maandalizi ya shughuli mbalimbali muhimu kuelekea mchakato huo wa kidemokrasia.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, watumishi wa umma wanaotarajia kugombea nafasi za kisiasa katika uchaguzi huo watapaswa kujiuzulu nyadhifa zao ifikapo Februari 9, 2027, sawa na miezi sita kabla ya siku ya uchaguzi kama inavyotakiwa na sheria.

IEBC pia imezitaka vyama vya siasa kuwasilisha orodha za wanachama wao pamoja na majina ya watakaoshiriki katika kura za mchujo kabla ya Machi 16, 2027. Vyama hivyo vitawajibika pia kuwasilisha ratiba na maeneo yatakayofanyika kura hizo za ndani.

Kwa mujibu wa tume hiyo, vyama vya siasa vinapaswa kukamilisha kura za mchujo na kutatua migogoro yote ya ndani kabla ya Mei 9, 2027. Vilevile, wagombea binafsi watakaotaka kuwania nafasi mbalimbali hawatapaswa kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa kufikia tarehe hiyo.

Katika ratiba hiyo, IEBC imeeleza kuwa kampeni rasmi za uchaguzi zitaanza Mei 29, 2027 na kumalizika Agosti 7, 2027, saa 48 kabla ya wananchi kuelekea kwenye vituo vya kupigia kura.

Tangazo hilo linaashiria kuanza rasmi kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu ambao utawachagua viongozi wa ngazi mbalimbali nchini Kenya, ikiwemo Rais, Wabunge, Magavana na wawakilishi wengine wa wananchi.

Leave a Comment