Wakenya wameeleza kutoridhishwa na kukasirishwa baada ya video kusambaa ikionyesha maafisa wa polisi wakimkamata kwa nguvu mwanamume mwenye ulemavu wakati wa maandamano ya kupinga serikali mjini Nakuru, yaliyofanyika jana Alhamisi.
Huduma ya Kitaifa ya Polisi ya Kenya imekosolewa vikali baada ya tukio hilo linalomhusisha James Thuku, ambaye hutumia magongo kutembea, kuonekana akivutwa na kuangushwa chini kabla ya kuingizwa kwenye gari la polisi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Seneta Crystal Asige, Thuku alikamatwa na anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Nakuru kwa tuhuma za kuchochea vurugu.
“Nimeweza kuthibitisha kwamba alikamatwa na anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Nakuru. Jina lake ni James Thuku. Mashtaka: kuchochea vurugu,” Seneta Crystal Asige aliandika kwenye mtandao wa X.
Seneta huyo ameitaka mamlaka ya polisi kutoa maelezo kuhusu mazingira ya kukamatwa kwake.
Video hiyo iliyosambaa mitandaoni inaonyesha Thuku akijaribu kuvuka barabara akiwa ameandamana na mtu mwingine wakati wa maandamano. Gari la polisi aina ya Land Cruiser kisha linafika eneo hilo likiwa na maafisa zaidi ya kumi waliokuwa na silaha na vifaa vya kudhibiti vurugu.
Baada ya maafisa hao kushuka, mtu aliyekuwa akimsaidia Thuku anakimbia, na kumwacha akiwa peke yake. Thuku anaanguka chini wakati akijaribu kukwepa kukamatwa kabla ya kuburutwa na maafisa hao na kisha kuwekwa ndani ya gari la polisi.
Tukio hilo limeibua ukosoaji mkali kutoka kwa wananchi na watumiaji wa mitandao ya kijamii, wengi wakilaani matumizi ya nguvu dhidi ya mtu mwenye ulemavu.
Wadau wa haki za binadamu wametoa wito wa uchunguzi huru kubaini iwapo taratibu za polisi zilizingatiwa na kama nguvu iliyotumika ilikuwa ya lazima katika tukio hilo.