
Dodoma – Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ametangaza marufuku ya mikutano yote ya vyama vya siasa nchini, ikiwemo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hadi pale itakapotolewa taarifa nyingine.
Katambi ametoa marufuku hiyo Leo, Juni 26, 2026 akizungumza Bungeni, Dodoma.
Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia tishio la uwepo wa maandamano kuelekea kilele cha Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Waziri Katambi amemwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillus Wambura, kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa kikamilifu na kutoruhusu mikutano yoyote ya kisiasa kufanyika hadi itakapotangazwa vinginevyo.
Aidha, amewataka wamiliki wa hoteli, nyumba za wageni (gesti) na nyumba za kulala wageni kuhakikisha wanawasajili wateja wao kwa kutumia vitambulisho vya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili kurahisisha utambuzi wa wageni na kuimarisha usalama.
Amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wamiliki wa maeneo ya malazi watakaobainika kutowasajili wageni wao kwa mujibu wa maelekezo hayo.