×

Meneja wa Zamani wa TRA Kigoma Ahukumiwa Miaka 20 Jela Kwa Kukutwa na Meno ya Tembo

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma imemhukumu kifungo cha miaka 20 gerezani aliyekuwa Meneja wa TRA Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma, Irving Bagasheki(40) baada ya kumkuta na hatia katika makosa mawili ya kujihusisha na nyara za serikali isivyo halali, ambazo ni meno mawili ya tembo yenye thamani ya shilingi milioni 52.

Hukumu hiyo imetolewa Juni 29, 2026 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma, Aristida Tarimo mbele ya Jopo la Mawakili wa Serikali lililoongozwa na Felix Kwetukia, baada ya Mahakama kujiridhisha kuwa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka ulithibitisha makosa hayo bila kuacha shaka yoyote.

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, Bagasheki (40) alikamatwa Julai 1, 2024 katika eneo la Beria ya Kihomoka, Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma akiwa ndani ya gari la serikali lenye namba za usajili STL 7274 akijaribu kusafirisha meno hayo mawili ya tembo kinyume na sheria za nchi.

Baada ya kukamatwa, yeye pamoja na watuhumiwa wengine watano walifikishwa mahakamani katika kesi namba 4733 ya mwaka 2025 wakikabiliwa na mashtaka ya kupatikana na nyara za Serikali isivyo halali na kujihusisha na nyara hizo.

Hata hivyo, Mahakama iliwachia huru Watuhumiwa wengine watano ambao ni Hosea Bwandu Ntakimulela, Mathias Kimanuka, Daniel Ezekiel Mbwambo, Ngendamenya Kagozi na Majid Husein Bidebe, baada ya kuridhika kuwa ushahidi haukuwa wa kutosha kuwahusisha na makosa hayo.

Katika hukumu yake, Mahakama ilimhukumu Bagasheki kifungo cha miaka 20 kwa kosa la kwanza la kupatikana na nyara za serikali isivyo halali na miaka 20 kwa kosa la pili la kujihusisha na nyara hizo. Hata hivyo, adhabu hizo zitaenda kwa pamoja, hivyo atatumikia kifungo cha miaka 20 gerezani. Makosa hayo yalikuwa chini ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyama Pori na Sheria ya Uhujumu Uchumi kama ilivyofafanuliwa katika hati ya mashtaka

Leave a Comment