
Nyota wa NBA LeBron James ameamua kuhitimisha safari yake ya miaka minane akiwa na Los Angeles Lakers, hatua inayofungua ukurasa mpya katika maisha yake ya soka la kikapu.
LeBron, mwenye umri wa miaka 41, anaondoka Lakers baada ya kuisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa wa NBA mwaka 2020 na kuwa mmoja wa wachezaji walioandika historia kubwa ndani ya kikosi hicho.
Kwa mujibu wa mwandishi wa ESPN, Shams Charania, uamuzi wa LeBron haujachochewa na fedha, bali umetokana na kutafuta furaha na mazingira mapya katika hatua hii ya mwisho ya maisha yake ya uchezaji.
“Huu ni uamuzi unaoongozwa na furaha. Popote atakapokwenda, haitakuwa kwa sababu ya pesa,” alinukuliwa Charania.
Kuondoka kwa LeBron pia kumeibua mjadala kuhusu nafasi yake ndani ya Lakers baada ya kuwasili kwa Luka Dončić, ambaye alichukua nafasi kubwa zaidi kama nyota wa kikosi. Hata hivyo, hakuna taarifa rasmi zinazoonyesha kuwa Dončić ndiye sababu ya LeBron kuondoka.
Kwa sasa, LeBron anatarajiwa kuingia kwenye soko la wachezaji huru (free agency), huku timu mbalimbali zikitajwa kuwa na nafasi ya kuwania saini yake. Wakati huohuo, mustakabali wa mwanawe Bronny James, ambaye bado ana mkataba na Lakers, unaendelea kuwa gumzo miongoni mwa mashabiki wa NBA.