
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeitoza Klabu ya Young Africans (Yanga SC) faini ya Sh. milioni 100 kwa kukiuka taratibu za matumizi ya chumba rasmi cha kuvulia katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya JKT Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa ya TPLB iliyotolewa Julai 3, 2026, adhabu hiyo inatokana na mchezo namba 233 uliochezwa Julai 2, 2026, ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
TPLB imesema wachezaji na maofisa wa ufundi wa Yanga walitumia nyumba iliyopo nje ya uwanja badala ya kutumia chumba rasmi cha kuvalia nguo kilichotengwa ndani ya uwanja, jambo ambalo linadaiwa kukiuka Kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Bodi hiyo imeeleza kuwa adhabu ya faini ya Sh. milioni 100 imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 27:7 ya Ligi Kuu kuhusu Vyombo vya Maamuzi.
TPLB imekumbusha kuwa mwezi Mei 2026, Yanga pia iliwahi kutozwa faini ya Sh. milioni 30 kwa kosa linalofanana la kutotumia chumba rasmi cha kuvulia na badala yake kutumia nyumba iliyo nje ya uwanja wa mchezo.
