×

Mke wa Obama Afichua Filamu Aipendayo Zaidi Duniani

Mke wa aliyekuwa Rais wa Marekani Barack Obama, Michelle Obama.

Mke wa aliyekuwa Rais wa Marekani Barack Obama, Michelle Obama amefunguka kuhusu filamu anayopenda zaidi duniani, akishangaza wengi baada ya kutaja kuwa anayoipenda sana ni ya vichekesho ya sikukuu “Elf” iliyotoka mwaka 2003.

Katika mahojiano kupitia podcast yake ya “IMO with Michelle Obama & Craig Robinson”, Michelle Obama alimkaribisha muigizaji nyota wa filamu hiyo Will Ferrell, ambaye aliigiza kama Buddy the Elf.

Michelle Obama alisema kuwa “Elf” ni filamu anayoweza kuitazama mara kwa mara bila kuchoka, akieleza kuwa ni ya kuchekesha, yenye hisia nzuri na inayomfanya ajisikie vizuri kila anapohitaji kuburudika.

Amesema filamu hiyo kwake imekuwa kama “dawa ya furaha”, na mara nyingi huichagua wakati anapohitaji kubadilisha mood yake au kujipa nguvu ya furaha.

Kwa upande wake, Will Ferrell alizungumzia safari ya kutengeneza filamu hiyo, akieleza jinsi alivyotoka kwenye kipindi cha Saturday Night Live na kuingia kwenye mradi wa “Elf” uliobadilika na kuwa moja ya filamu kubwa za sikukuu duniani.

Ferrell alisema hakuwahi kufikiria kama filamu hiyo ingekuwa na mafanikio makubwa kiasi hicho, lakini hatimaye imekuwa moja ya kazi zake zinazopendwa zaidi duniani.

Kauli ya Michelle Obama imezua mjadala mtandaoni huku wengi wakishangaa uchaguzi wake wa filamu, lakini pia wengi wakikubaliana kuwa “Elf” ni moja ya classics zinazopendwa na familia nyingi duniani.

Leave a Comment