
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Munisi, amesema ushirikiano wa karibu kati ya waajiri, wafanyakazi na vyama vya wafanyakazi ni nguzo muhimu katika kujenga mazingira bora ya kazi na kupunguza migogoro sehemu za kazi.
Mhe. Dkt. Munisi ameyasema hayo Julai 2, 2026, alipotembelea Kampuni ya Société Générale de Surveillance (SGS) iliyopo Nyegezi, mkoani Mwanza, kwa lengo la kukagua utekelezaji wa masuala ya kazi, ajira na mahusiano kazini.
Aidha, amewataka waajiri na wafanyakazi kuendelea kushirikiana na Maafisa Kazi wa Mikoa ili kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu za ajira zinafuatwa, hatua ambayo itasaidia kuimarisha amani na tija katika maeneo ya kazi.

Dkt. Munisi pia amesisitiza utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kuhusu kima cha chini cha mshahara, akiwataka waajiri ambao bado hawajaanza kulipa viwango vilivyowekwa kufanya hivyo mara moja kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Serikali chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwajali na kuwathamini wafanyakazi ili kuhakikisha kila Mtanzania anafanya kazi katika mazingira yenye staha na usalama.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kamishna Msaidizi wa Ukaguzi Amesema ushirikiano kati ya waajiri, wafanyakazi, vyama vya wafanyakazi na Maafisa Kazi unarahisisha utekelezaji wa sheria na huchangia kupunguza migogoro, kuongeza tija na kujenga mazingira bora ya kazi nchini.
Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni ya SGS Omari Ngereza ameishukuru Serikali kwa ziara hiyo na ushauri uliotolewa na Kuahidi kutekeleza maelekezo yote waliopokea.
Huku mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo, Bi. Jackline Michael, akiishukuru Serikali kwa kuendelea kusimamia haki na ustawi wa wafanyakazi, hatua ambayo amesema imeongeza ari ya kazi na kuimarisha mahusiano mema mahali pa kazi.