
Dodoma, Julai 5, 2026 – Mamilioni ya wakulima nchini yanatarajiwa kunufaika na huduma za kifedha za kidijitali kufuatia kuendelezwa kwa makubaliano ya ushirikiano kati ya kampuni ya MIXX na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), yanayolenga kuimarisha uwazi, ufanisi na upatikanaji wa huduma za kifedha kupitia teknolojia.
Makubaliano hayo yanalenga kuboresha usimamizi wa fedha katika vyama vya ushirika, kuongeza uwajibikaji, pamoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kifedha kwa wanachama.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Prof. Peter Msoffe, alisema biashara zinazofanyika kupitia vyama vya ushirika zina thamani inayokadiriwa kufikia kati ya Sh trilioni 5 hadi 7, hali inayovifanya vyama hivyo kuwa nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara wa MIXX, James Sumari, alisema ushirikiano huo utasaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kifedha kwa wakulima na vyama vya ushirika.
“Tunataka vyama vya ushirika viweze kusimamia fedha zao kwa uwazi na kuwafikishia wanachama huduma za kifedha kwa urahisi zaidi. Hii itasaidia kuongeza tija na kuchochea maendeleo ya uchumi wa wananchi,” alisema Sumari.
Alieleza kuwa kupitia mfumo wa Mixx Kikoba, vyama vya ushirika vitaweza kusimamia michango, kufanya malipo, kununua hisa, kupokea gawio na kuomba mikopo kwa kutumia simu za mkononi.
Sumari aliongeza kuwa kupitia jukwaa la Mixx Kilimo, zaidi ya wakulima 300,000 tayari wamefikiwa na huduma za kifedha, huku zaidi ya Shilingi bilioni 700 zikiwa zimepitishwa katika sekta ya kilimo ndani ya kipindi cha miaka sita iliyopita.
Naye Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege, alisema matumizi ya teknolojia ni nguzo muhimu katika kuimarisha sekta ya ushirika na kuongeza uwazi katika usimamizi wa fedha.
“Serikali inaendelea kuhimiza matumizi ya teknolojia ili kuongeza uwazi na ufanisi katika vyama vya ushirika. Ushirikiano huu utasaidia kuwajengea uwezo viongozi na wanachama kupata huduma bora za kifedha,” alisema Dkt. Ndiege.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kuongeza matumizi ya huduma rasmi za kifedha kwa wakulima, kuboresha utendaji wa vyama vya ushirika na kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa Taifa.