
Mvutano kati ya Iran na Marekani umeongezeka tena baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) kudai kushambulia vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Bahrain na Kuwait kwa makombora na droni, kufuatia mashambulizi mapya ya Marekani dhidi ya malengo ya kijeshi ya Iran.
Kwa mujibu wa IRGC, operesheni hiyo ililenga kituo cha jeshi la majini cha Marekani kilichopo Bahrain pamoja na Kituo cha Anga cha Ali Al Salem nchini Kuwait. Iran pia ilidai kuidungua droni ya Marekani aina ya MQ-9 Reaper iliyokuwa ikifuatilia operesheni hiyo. Kufuatia mashambulizi hayo, ving’ora vya tahadhari ya mashambulizi ya anga vilisikika nchini Bahrain na Kuwait.
Jeshi la Kuwait lilisema mifumo yake ya ulinzi wa anga ilikuwa ikikabiliana na mashambulizi ya makombora na droni, huku Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ikithibitisha kuwa ilikuwa imefanya mashambulizi dhidi ya zaidi ya boti 60 ndogo za IRGC pamoja na mifumo ya ulinzi wa anga, makombora ya pwani, vifaa vya ufuatiliaji na maeneo ya kurushia droni nchini Iran.
CENTCOM ilisema hatua hiyo ilichukuliwa kujibu mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara katika Mlango wa Hormuz, ikieleza kuwa vitendo vya Iran vinakiuka makubaliano ya kusitisha mapigano na kuhatarisha uhuru wa usafiri wa baharini.
Kwa upande wake, makao makuu ya kijeshi ya Iran ya Khatam Al-Anbiya yalilaani mashambulizi ya Marekani, yakiyaita “uchokozi wa wazi,” na kuahidi kutoa jibu kali huku yakisisitiza kuwa Tehran haitaruhusu kuingiliwa katika usimamizi wa Mlango wa Hormuz.
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, aliishutumu Marekani kwa kuvunja makubaliano ya usitishaji mapigano kupitia mashambulizi mapya ya kijeshi, kurejesha vikwazo vya mauzo ya mafuta ya Iran na hatua nyingine za kijeshi katika eneo hilo.
Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Iran viliripoti milipuko katika maeneo ya Kisiwa cha Kharg, Qeshm, Sirik na Bandar Abbas, huku watu kadhaa wakijeruhiwa baada ya mabaki ya kombora kuangukia katika eneo la bandari ya Sirik. Hakukuwa na taarifa za vifo vya raia.
Meli za Mafuta Zabadilisha Njia Hormuz
Mvutano huo pia umeathiri usafirishaji wa nishati duniani baada ya angalau meli nne za mafuta na gesi kubadili njia na kuacha kuvuka Mlango wa Hormuz kutokana na hofu ya usalama.
Meli tatu za gesi asilia za QatarEnergy pamoja na tanker moja iliyokuwa imebeba mapipa milioni mbili ya mafuta ghafi kutoka Kuwait zilirejea nyuma kabla ya kuingia katika mlango huo muhimu wa bahari.
Hatua hiyo ilifuatia mashambulizi dhidi ya tanker ya gesi ya Qatar na tanker ya mafuta ya Saudi Arabia yaliyoripotiwa kutokea karibu na Hormuz, hali iliyosababisha mamlaka za usafiri wa baharini kuongeza kiwango cha tahadhari kwa meli zinazopita katika eneo hilo.
Bei ya Mafuta Yapanda
Bei ya mafuta duniani iliongezeka kwa zaidi ya asilimia tatu baada ya Marekani kutangaza kufuta kibali kilichokuwa kinaruhusu Iran kuuza mafuta katika soko la kimataifa.
Iran imeelezea hatua hiyo kuwa ni ukiukaji wa makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano na kuonya kuwa itachukua hatua zote muhimu kulinda maslahi na usalama wake wa taifa.
Mvutano huo unaendelea kutishia makubaliano ya muda yaliyofikiwa mwezi uliopita kati ya Tehran na Washington, huku mazungumzo ya kufikia makubaliano ya kudumu yakikwama na hatari ya kurejea kwa mapigano makubwa ikiendelea kuongezeka.