×

Godbless Lema Avunja Ukimya Mjadala wa Degree na Kufua Boxer

Mwanasiasa Godbless Lema

Kufuatia mjadala uliosambaa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kauli ya mtumishi wa Mungu Rose Shaboka kuhusu mwanamke mwenye shahada nyingi kuishia kuwa mke anayefua nguo za mume wake na kupika, mwanasiasa Godbless Lema ametoa mtazamo wake akisisitiza kuwa ndoa haipaswi kuonekana kama kikwazo cha ndoto za mtu binafsi.

Lema amesema changamoto ya zama hizi ni kwamba wakati mwingine ndoa huwasilishwa kana kwamba ni gereza la ndoto, ilhali ndoa yenye afya ni mahali ambapo ndoto za pande zote mbili zinaweza kukua na kustawi. Amesema pamoja na ndoto hizo zote, lengo kuu linapaswa kuwa kuishi kwa upendo, furaha, heshima na unyenyekevu.

Ameeleza kuwa kufua boxer, kupika au kushiriki kazi nyingine za nyumbani ukiwa na shahada nyingi si udhaifu, kama ambavyo elimu si kipimo cha ubora wa ndoa wala thamani ya mtu. Kwa mujibu wake, elimu na huduma vinaweza kwenda pamoja bila mgongano.

“Elimu haimfanyi mtu kuwa mkubwa kuliko huduma, na huduma haipunguzi hadhi ya mtu. Mtu anaweza kuwa na shahada nyingi, akaongoza taasisi, akaleta mabadiliko makubwa katika jamii, na bado akachagua kutenda kwa upendo ndani ya familia yake. Huko si kushushwa hadhi, bali ni uchaguzi wa upendo na uwajibikaji,” amesema.

Mtumishi wa Mungu Rose Shaboka

Aidha, Lema amesema tatizo huanza pale majukumu ya kifamilia yanapoonekana kama adhabu badala ya fursa ya kujitoa kwa ajili ya familia. Amefafanua kuwa ndoa si mashindano ya vyeo, mishahara au vyeti, bali ni safari ya kuulizana kila siku, “Leo nifanye nini ili maisha yetu yawe bora zaidi?”

Amesisitiza kuwa ingawa ndoto za kila mmoja zina thamani, ndoa yenye afya hujengwa pale ambapo “sisi” inakuwa kubwa kuliko “mimi”. Kwa maoni yake, wakati mwingine mmoja anaweza kuahirisha au kurekebisha baadhi ya mipango yake kwa ajili ya ustawi wa familia, jambo ambalo si udhaifu bali ni ishara ya ukomavu na kujitoa.

Lema ameongeza kuwa swali la msingi halipaswi kuwa nani afue boxer au apike, bali kama wanandoa wanajenga maisha yanayompa kila mmoja nafasi ya kutimiza ndoto zake huku wakilinda upendo, amani na heshima ya pamoja.

Kwa mujibu wake, ndoa haijengwi na shahada, cheo au mafanikio ya nje, bali hujengwa na upendo, heshima, unyenyekevu na kujitoa. Amesema mwanamke hapaswi kuzuiwa kukua katika elimu, taaluma na maarifa, huku mwanaume naye akipaswa kuendelea kukua katika wajibu, busara na upendo ili wote wawili wajenge familia imara.

Akihitimisha, Lema amesema huenda hoja ya Rose Shaboka ilikuwa na msingi, lakini namna ilivyowasilishwa ndiyo iliyozua mjadala mkubwa. Amesema masuala nyeti yanahitaji kuwasilishwa kwa unyenyekevu, busara na maarifa ili kuepusha tafsiri zinazoweza kupotosha maana halisi ya ujumbe.

Leave a Comment