
NAJAF, Iraq: Maelfu ya waombolezaji walijitokeza Jumatano katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kushiriki msafara wa mazishi ya aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, huku jeneza lake likiendelea na safari ya siku sita ya kuagwa baada ya kuvuka mpaka kutoka Iran.
Waombolezaji waliokuwa wamebeba picha kubwa za Khamenei walijipanga kando ya barabara huku wakipaza sauti kauli za kupinga Marekani na Israel wakati gari lililobeba jeneza lake likipita katika mitaa ya Najaf.
Bendera za Iraq na Iran zilionekana zikipepea pamoja na bendera za makundi ya wanamgambo wa Iraq yanayoungwa mkono na Iran, huku wafuasi wao wakijiunga na maelfu ya watu waliohudhuria msafara huo.

Mji wa Najaf una umuhimu mkubwa kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia duniani, kwani ndipo alipozikwa Imam Ali, binamu na mkwe wa Mtume Muhammad (SAW).
Jeneza la Khamenei liliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Najaf Jumanne jioni Julai 7, 2026 ambapo lilipokelewa na Waziri Mkuu wa Iraq, Ali al-Zaidi, viongozi waandamizi wa serikali pamoja na viongozi wa kidini.
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, pamoja na makamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), pia walihudhuria msafara huo wa mazishi.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa, msafara huo utaendelea kuelekea mji mtakatifu wa Karbala kabla ya mwili wa Khamenei kurejeshwa nchini Iran kwa ajili ya mazishi ya mwisho.
Khamenei aliuawa Februari 28 katika mashambulizi ya anga yaliyotekelezwa na Israel na Marekani, tukio lililozidisha mvutano mkubwa katika Mashariki ya Kati na kuibua maombolezo makubwa nchini Iran na miongoni mwa washirika wake katika ukanda huo.




