×

Nyota wa Kombe la Dunia Jayden Adams Afariki Ghafla

Soka la Afrika Kusini limegubikwa na majonzi kufuatia kifo cha kiungo wa Mamelodi Sundowns na timu ya taifa ya Afrika Kusini (Bafana Bafana), Jayden Adams, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 25, wiki chache tu baada ya kushiriki Kombe la Dunia la FIFA 2026.

Adams, ambaye aliichezea Afrika Kusini katika mechi mbili za mwanzo za Kombe la Dunia, alikuwa miongoni mwa wachezaji walioisaidia nchi hiyo kuweka historia ya kufuzu hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza katika mashindano hayo.

Habari za kifo chake zimeishtua familia ya soka, huku klabu yake ya zamani ya Stellenbosch FC, Mamelodi Sundowns, wachezaji wenzake na mashirika mbalimbali ya soka wakitoa salamu za rambirambi na kueleza masikitiko yao makubwa.

Chama cha Wachezaji wa Soka Afrika Kusini (SAFPU) kilisema kimepokea kwa huzuni taarifa za kifo cha Adams, kikimtaja kuwa mchezaji mwenye kipaji kikubwa aliyeiwakilisha nchi yake kwa heshima, ujasiri na kujituma.

Stellenbosch FC, ambako Adams alianza safari yake ya soka la kulipwa akiwa na umri wa miaka 19, ilisema ameacha historia kubwa ndani ya klabu hiyo baada ya kucheza mechi 139 na kusaidia timu kutwaa ubingwa wa Carling Knockout mwaka 2023.

Mwaka 2025 alijiunga na Mamelodi Sundowns, ambako aliendelea kung’ara na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League).

Wachezaji wenzake nao walieleza huzuni kupitia mitandao ya kijamii. Gomolemo Kekana alisema amevunjika moyo, huku Aubrey Modiba na Keanu Cupido wakishindwa kuficha maumivu yao kutokana na msiba huo.

Kifo cha Adams kinakuja siku chache baada ya familia yake kukumbwa na msiba mwingine, kufuatia bibi yake, Marianna Adams, kufariki dunia wakati akiwa kambini na timu ya taifa kwenye Kombe la Dunia. Licha ya kupokea taarifa hizo za huzuni, Adams aliendelea kuichezea Afrika Kusini katika mechi dhidi ya Czechia na baadaye akachangia ushindi dhidi ya Korea Kusini ulioiwezesha timu hiyo kufuzu hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza katika historia yake.

Hadi sasa, chanzo cha kifo cha Jayden Adams hakijatangazwa rasmi.

Leave a Comment