
Kiongozi Mkuu wa Iran, Mojtaba Khamenei, ametishia kulipiza kisasi kwa kifo cha mtangulizi wake na baba yake, Ayatollah Ali Khamenei, akisema hatua hiyo haitatekelezwa na Iran pekee bali pia kwa ushirikiano wa watu wote wanaojiona kuwa huru duniani.
Katika ujumbe wake wa kwanza kwa umma tangu kuanza kwa shughuli za mazishi ya baba yake wiki iliyopita, uliorushwa na televisheni ya taifa, Mojtaba alisema kulipiza kisasi ni matakwa ya taifa la Iran na kwamba lazima kutekelezwe.
Ayatollah Ali Khamenei aliuawa katika shambulio la anga lililodaiwa kufanywa kwa ushirikiano wa Marekani na Israel mnamo Februari 28, mwanzoni mwa vita vilivyozuka kati ya pande hizo.
“Tunaahidi kulipiza damu ya kiongozi wetu shujaa pamoja na mashujaa wote waliopoteza maisha katika vita hivi viwili dhidi ya wauaji wahalifu na waliovunjika heshima,” sehemu ya taarifa hiyo ilisema.
Mojtaba Khamenei, ambaye kwa mujibu wa vyanzo vya ngazi za juu alipata majeraha usoni pamoja na majeraha mengine katika shambulio hilo, hajaonekana hadharani tangu alipoteuliwa kuwa Kiongozi Mkuu wa Iran Machi 8.
Katika ujumbe wake, alisema kuwa hata kama yeye hatakuwepo, kisasi hicho kitatimizwa, akisisitiza kuwa watu huru duniani watashiriki kutekeleza kile alichokiita jukumu la kimungu.
Wakati huohuo, mashambulizi mapya kati ya majeshi ya Marekani na Iran yaliyotokea wiki hii yamezua mashaka kuhusu hatima ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kati ya Washington na Tehran kwa lengo la kumaliza vita vilivyodumu kwa miezi minne. Iran inaamini makubaliano hayo yataisaidia nchi hiyo kupata manufaa makubwa ya kiuchumi.
Licha ya mvutano huo, Rais wa Marekani Donald Trump alisema Ijumaa kuwa, ingawa usitishaji mapigano umevunjika, Marekani na Iran zimekubaliana kuendelea na mazungumzo.
Kutokuwepo kwa Mojtaba Khamenei mbele ya umma tangu kushika madaraka kumeendelea kuzua maswali miongoni mwa Wairani, huku baadhi wakisema ni muhimu aonekane hadharani hata kama bado anaendelea kuuguza majeraha aliyoyapata.
Ayatollah Ali Khamenei, aliyeiongoza Iran kwa miaka 37, alizikwa katika eneo takatifu zaidi nchini humo baada ya mamia ya maelfu ya waombolezaji kuhudhuria mazishi yake, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.