×

FIFA Yaanza Kuuza Vipande vya Nyasi za Uwanja wa Fainali ya Kombe la Dunia 2026

Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeanzisha mauzo ya vipande vya nyasi halisi vitakavyotumika kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Dunia 2026, hatua iliyozua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa soka duniani.

FIFA inauza kila kipande cha nyasi kwa dola za Marekani 450 (zaidi ya shilingi milioni moja za Tanzania), huku nyasi hizo zikitoka katika uwanja wa MetLife Stadium uliopo New Jersey, Marekani, ambako fainali ya Kombe la Dunia itachezwa Julai 19.

Kwa mujibu wa duka rasmi la FIFA, kila kipande cha nyasi kimehifadhiwa ndani ya kifaa maalumu cha akriliki (acrylic) pamoja na kifaa cha kumbukumbu cha USB chenye alama ya uthibitisho wa uhalisia wake. Bidhaa hiyo pia imefungashwa kwenye boksi maalumu kwa ajili ya wakusanyaji wa kumbukumbu na mashabiki wa soka.

FIFA imeeleza kuwa bidhaa hiyo inalenga kuwapa mashabiki nafasi ya kumiliki sehemu ya historia ya mojawapo ya matukio makubwa zaidi ya michezo duniani. Hata hivyo, shirika hilo halijafafanua iwapo vipimo vilivyotajwa vya kipande hicho (17.5 x 17.5 x 17.5) ni kwa inchi, sentimita au milimita.

Bidhaa hiyo itapatikana kwa usafirishaji ndani ya Marekani na Ulaya pekee, huku oda zote zikitarajiwa kutumwa baada ya fainali ya Kombe la Dunia kumalizika.

Tangazo hilo limekuja wakati FIFA ikiendelea kukosolewa kutokana na gharama kubwa za tiketi za mashindano hayo. Bei ya tiketi za kawaida za fainali imefikia hadi dola 32,970 ( Sawa na milioni 85.7 za Tanzania) , huku tiketi za huduma maalumu (hospitality) zenye chakula na vinywaji zikiuzwa kwa dola 34,500 (milioni 89.7) na dola 32,500 (milioni 84.5).

Leave a Comment