
Muigizaji maarufu wa New Zealand, Sam Neill, aliyepata umaarufu mkubwa duniani kupitia nafasi yake ya Dk. Alan Grant katika filamu za “Jurassic Park”, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 78.
Familia yake ilithibitisha taarifa hiyo Jumatatu kupitia taarifa iliyotolewa kwenye mitandao ya kijamii, ikisema Neill alifariki akiwa amezungukwa na familia yake.
“Sam alikuwa pamoja na familia yake na amefariki kwa utulivu na heshima iliyotambulisha maisha yake yote,” familia ilisema.
Aidha, familia ilieleza kuwa kifo chake kilikuwa cha ghafla na kisichotarajiwa, lakini ikabainisha kuwa wakati wa kifo chake hakuwa tena na saratani.

Neill alikuwa ametangaza mwezi Aprili mwaka huu kuwa alikuwa amepona saratani ya damu baada ya kutumia takriban miaka mitano akipatiwa matibabu.
Muigizaji huyo alipata umaarufu wa kimataifa mwaka 1993 alipocheza nafasi ya Dk. Alan Grant katika filamu ya “Jurassic Park”, na baadaye alirejea kuigiza nafasi hiyo katika filamu nyingine za mfululizo huo, na kuwa mmoja wa wahusika waliopendwa zaidi na mashabiki wa filamu hizo duniani.
Kifo chake kimeacha pengo kubwa katika tasnia ya filamu duniani, huku mashabiki na wadau wa burudani wakimkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika uigizaji na urithi aliouacha kupitia kazi zake maarufu.
