×

Nusu Fainali ya Moto! Konate wa Ufaransa Afungaka Kabla ya Kukutana na Hispania Kesho

Beki wa timu ya taifa ya Ufaransa, Ibrahima Konate

Beki wa timu ya taifa ya Ufaransa, Ibrahima Konate, amesema hawana hofu ya kukutana na Hispania katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia 2026, lakini wanaiheshimu kutokana na kiwango bora ilichokionyesha katika mashindano hayo.

Ufaransa itakutana na Hispania kesho, Julai 14, 2026 saa nne usiku, katika mchezo unaotarajiwa kuwa wa ushindani mkubwa huku timu zote zikiwa zinawinda nafasi ya kucheza fainali ya dunia.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumapili, Konate amesema hakuna sababu ya kuiogopa timu yoyote katika hatua hii ya mashindano, huku akisisitiza kuwa Ufaransa itajiandaa kwa umakini mkubwa ili kupata matokeo mazuri.

“Huwezi kumuogopa mpinzani yeyote. Tutajiandaa vizuri kadri tuwezavyo na tunatumaini matokeo yatakuwa upande wetu,” alisema Konate.

Hispania imefika hatua hiyo ikiwa imeruhusu bao moja pekee katika michuano yote ya Kombe la Dunia 2026, huku ikiendelea kusaka taji lake la pili la dunia.

Konate ameisifu Hispania kwa kuwa na kikosi chenye vipaji vingi, akisema Ufaransa haitafanya kosa la kumlenga mchezaji mmoja pekee, licha ya kiwango bora kinachoendelea kuonyeshwa na nyota wao Lamine Yamal.

“Hispania ni timu ya kipekee yenye wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa. Hatutakuwa tunamfikiria Lamine Yamal pekee, ingawa ni mchezaji bora,” aliongeza.

Ufaransa, ambayo ilitwaa Kombe la Dunia mwaka 2018 na kumaliza nafasi ya pili mwaka 2022, ina kumbukumbu ya kukutana na Hispania katika mechi kubwa za hivi karibuni, ikiwemo kufungwa katika nusu fainali ya Euro 2024 na pia kwenye Nations League mwaka uliopita.

Endapo Ufaransa itaifunga Hispania na kufuzu fainali itakayochezwa Julai 19 jijini New York, itakuwa imefikia fainali ya tano ya Kombe la Dunia katika historia yake, hatua itakayozidi kuimarisha nafasi yake kama moja ya mataifa makubwa zaidi katika soka la dunia.

 

Leave a Comment