
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimeeleza kutoridhishwa na kauli ya Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, kwa kutaja baadhi ya ajenda zinazodaiwa kuwa sehemu ya vikao vya pamoja kati ya vyama hivyo viwili.
CCM imesema hatua hiyo inaweza kuathiri mchakato wa mazungumzo na nia njema iliyopo katika kutafuta masuala ya pamoja kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, amesema ni muhimu pande zote kuheshimu usiri wa vikao, kanuni, maadili na miiko iliyokubaliwa.
Mbeto amesema si sahihi kwa chama chochote kutangaza hadharani mambo yanayohusu ajenda za vikao ambavyo bado havijajadiliwa na kamati maalumu ya pamoja.
Amesema hadi sasa kilichofikiwa ni kusainiwa kwa tamko la pamoja ambalo limefungua njia ya kuanza majadiliano ya masuala mbalimbali kupitia kamati itakayoundwa na kupewa hadidu za rejea.
“Ni lazima viongozi wa pande zote mbili wawe na kaba ya usiri unaozingatia miiko na maadili yaliyokubaliwa. Upande wowote unapokiuka rejea za makubaliano unaweza kudhoofisha njia safi na dhamira njema,” alisema Mbeto.
Katibu huyo amesema wajumbe wa kamati ya pamoja ndio watakaopokea na kujadili ajenda mbalimbali, hivyo viongozi wa vyama wanapaswa kusubiri mchakato huo badala ya kutoa taarifa ambazo bado hazijafikia hatua ya maamuzi.
Mbeto pia amemtaja Othman Masoud kuwa alikosea kutaja baadhi ya ajenda katika mkutano na wanachama wa ACT Wazalendo uliofanyika Ukumbi wa Mpiga Dili, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini, Zanzibar.
Amesisitiza kuwa tamko la pamoja lililosainiwa kati ya pande hizo mbili si uamuzi wa upande mmoja wala halipaswi kutumiwa kama kauli ya kisiasa ya chama kimoja.
“Tamko la pamoja si uamuzi wala matakwa ya upande mmoja. Jambo hili ni nyeti na limebeba matumaini ya wananchi,” alisema.
Mbeto amesema mchakato huo unatokana na juhudi za mazungumzo yaliyodumu kwa takribani miezi minane, hivyo viongozi wanapaswa kuupa nafasi na kuepuka kugeuza suala hilo kuwa mjadala wa kisiasa.
Ameongeza kuwa hatua iliyopo sasa ni mwanzo wa mchakato huo na kila upande unapaswa kuwa makini ili kulinda lengo la mazungumzo hayo.